Karibu kwenye Msikiti Mkuu
Msikiti Mkuu upo Kilwa Kisiwani, kisiwa kidogo kilichopo kwenye pwani ya mashariki ya Tanzania. Takriban kiilomita 300 kusini mwa Dar es Salaam. Msikiti huu ambao umejengwa kwa maweni ni msikiti wa kale zaidi ulio imara Kusini mwa jangwa la Sahara. Magofu ya Kilwa Kisiwani na Mago Songo Mnara, Kisiwa cha jirani ni sehemu ya Urithi wa Utamaduni wa Dunia wa UNESCO. Visiwa hivi vilikuwa bandari muhimu kwenye njia za biashara za Bahari ya Hindi. Ingawa Kilwa Kisiwani inajulikana zaidi kupitia magofu, bado kuna jamii hai inayoishi katika kisiwa. Kwenye ziara nzima, utasikia kupitia makundi mbalimbali ya watumishi wanaofanya kazi kwenye Magofu ya Kilwa Kisiwani au ni wanajamii wa kisiwani.
Stop 1. Historia ya kina na yenye safu
Eneo hii inajumuisha misikiti miwili. Msikiti wa awali ambao ulijengwa katika karne ya 9 hadi ya 11 na upanuzi uliongezwa wakati wa kilele cha maendeleo ya kisiwa hicho katika karne ya 13 hadi 14. Matumizi na muundo wa usanifu wa upanuzi wa msikiti ni ushahidi wa mchango mkubwa ambao Kilwa Kisiwani iliutoa kwenye njia ya biashara ya Bahari ya Hindi, kuenea kwa tamaduni za Kiswahili, na Uislamu katika Afrika Mashariki. Mnamo karne ya 16, kisiwa kilivamiwa na Wareno na msikiti ukawa hautumiki tena. Baada ya hapo, udongo ulijaza msikiti na ukafunikwa hadi kwenye kuba. Uko hivi baada ya Neville Chittick (mtaalamu wa Uingereza na mtaalamu wa akiolojia) aliongoza uchimbaji wa kuuuibua Msikiti Mkuu kati ya 1958 hadi 1965, ndipo uliporejeshwa na kutumika tena.
Revocatus Weja Bugumba
Mimi kwangu msikiti mkuu ni taa au ni alama ya urithi wetu mkuu katika nchi yetu kwa sababu umeiongezea thamani eneo hili, kwa kuwa kwanza urithi wa taifa na pia kwa urithi wa Ulimwengu. Moja wapo ya sababu za kuingizwa eneo hili katika urithi wa dunia ni kuwa na majengo yenye usanifu bora na wa kisasa na ambao umetumia akili kubwa sana. Na pia uhaba wake au kutokuwepo katika maeneo mengine katika dunia kwa mfano msikiti mkuu sifa yake kubwa kama wengine wanavyoeleza ni kwamba umekuwa ni msikiti mkubwa kuliko yote Kusini mwa jangwa la Sahara kabla ya karne ya 16 na sifa yake kwamba ni msikiti ambao umeishi kwa miaka mingi karibu miaka 700, zimetumika 700, kwa hiyo sidhani kama kuna msikiti wowote Tanzania umetumia miaka 700 mfululizo
Mercy Mbogelah
Msikiti mkubwa una stori kubwa, tukianzia karne ya kumi na moja wakati unajengwa msikiti mdogo, na kwa karne zingine kama karne ya kumi na tatu, kumi na nne, wakati wanaendelea kufanya upanuzi ujenzi mkubwa kwenye msikiti. Hadithi kubwa ambayo nimesikia kuhusiana na msikiti mkubwa, ni kwamba ni msikiti mkubwa na mkongwe mpaka karne ya kumi na sita ndio ulikuwa msikiti mkubwa zaidi kwenye ukanda wa pwani Afrika Mashariki, ukilinganishwa na misikiti mingine mikongwe. Lakini zaidi sana hadithi ambayo nimeipenda zaidi kwenye msikiti mkubwa, ni stori ya Ibni Batuta ambaye huyu ni mtu maarufu msomi maarufu wa zamani, ambaye alifika Kilwa na alikaribishwa na sultani wakautumia msikiti mkubwa katika swala.
Masoudi Issa Abeid
Eneo la Kisiwani sasa hivi lina umuhimu mkubwa na lina maana kubwa sana, Kwa sababu hata Kilwa yenyewe yote imebebwa na hii Kilwa Kisiwani. Ukiangalia yani rasilimali zilizokuwepo hapa zote ndio inaibeba Kilwa mzima, ikapata jina kubwa na hata likapata matangazo ya umoja wa mataifa na urithi wa dunia, Kilwa mzima umeubeba Kilwa Kisiwani kwa hivyo ina umuhimu sana eneo hili.
Abdalla Ahmadi
Msikiti mkuu ulijengwa katika nyakati kombele, muda wa kwanza ni katika karne ya kumi, kumi na moja. Wa pili, katika karne ya kumi na tatu, kumi na nne, kumi na tano. kwa nini hasa, uwe msikiti mmoja kwa mawili, au ujengewe katika nyakati mbili? Kwa sababu Kilwa Kisiwani pekee walijenga misikiti tisini na tisa, kama majina ya Mwenyezi Mungu, ni siri kubwa. Kwa hio kwa huu msikiti wa kwanza uliojengwa katika karne ya kumi, kumi na moja ilikuwa hawatoshelezi katika zile ibada ya Ijumaa na Idi, ndipo wakaongezea ingine wakawa wanafanya ibada kwa wakati mmoja.
Stop 2. Kutakaswa kabla ya ibada
Kama ulivyo utaratibu wa sasa, yeyote aingiaye msikitini lazima kwanza apitie eneo la kutawaza. Ni eneo rasmi kwa ajili ya kujitakasa na kujisafisha kabla ya kuingia msikitini. Wafanyabiasha wa kiislamu na wanajamii walipitia eneo kwa ajili ya maandalizi ya ibada. Eneo la kutia udhu katika msikiti wa zamani ni sehemu pekee kwa ajili ya kijitakasa na kujisafisha kabla ya kuingia msikitini. Maji yalipatikana katika visima karibu na eneo la kutilia udhu. Katika eneo hilo kulikuwa na mawe kwa ajili ya kukaushia miguu na kisha kuomba dua fupi kabla ya kuingia msikitini kwa ajili ya ibada.
Masoudi Issa Abeid
Msikiti mkubwa ninapotembelea najiskia hali ya furaha sana, lakini vilevile bado kichwa changu muda mwingine kinanipa tena ndoto kufahamu jinsi ya ule msikiti jinsi ulivyojengwa mpaka sasa hivi, kwa mfano labda swali hilo litakuja baadaye, kwa mfano labda maeneo yale ya kutawazia maji kule kwenye kuchukua udhu kule, pale kuna mawe yanaweza yakafika tani tano, mpaka tani nne, lakini sasa yale mawe yanapatikana maeneo ya bara, kwa wakati huo hakuna teknolojia ya magari, au teknolojia yeyote ya kisasa, yalikuwa mawe yanakuja na nini, ukienda kule utayaona, na mpaka sasa hivi sio kusema labda uyatafute, utayaona, na mpaka sasa hivi mandhari yake mazuri kabisa. Na kwa hivyo hata mimi nikitembelea pale, napenda kila mara niangalie tu vitu vilivyofanyika kwa wakati huo, na vilikuwa hakuna teknolojia ya kisasa, ilikuwaje? Kwa hivyo utayakuta yale mawe yana ushahidi pale. Jiwe moja linafika tani nane, tani saba, lakini limekuja pale na mawe yote yale yanapatikana bara sio pwani, pwani zinapatikana jiwe la matumbawe, mto wa matumbawe, ambazo ni laini unaweza ukakata kwa msumeno ukafanyia ukarabati lakini yale ni mawe magumu.
Mzee Said Hamisi
Linatofautiana kidogo, linatofautiana kwa sababu ya sasa hivi tuseme teknolojia imeongezeka kidogo, unaweza kuta sasa hivi wameeka bomba, lakini zamani ilikuwa hakuna vitu kama hizo. Walikuwa wanatumia hizi kata za kuchota... Lakini zamani walikuwa wanaeka bomba zile za kupitisha maji ambazo za kujengwa moja kwa moja, Zinajengwa zinaingiza maji pale birikani watu waweze kuyatumia. Unaweza kuta kisima kiko huko, lakini kukawa na mfereji wa kuingiza maji hapa eneo la kuchukua. Lakini sasa hivi kuna koki zile watu wanafungua tu ni utaalamu tu kuongezeka.
Abdalla Ahmadi
Kwenye eneo la msikiti mkuu ukiwa lipo eneo la udhu, umuhimu mkuu huwezi kuingia ndani ya msikiti ili kufanya ibada, lazima uweze kuweka udhu ina maana kuweka udhu kutawaza, kisha unaingia ndani kwa ajili ya kufanya ibada. Kwa hivyo pale unakuwa upo katika hali ya usafi, kwa hivyo ina maana ni moja ikawekwa sehemu ya kutawaza, kuingia ndani kwa ajili ya kufanya ibada, kwa hivyo lina umuhimu zaidi.
Stop 3. Kuchunguza msikiti wa asili
Jengo hili ni "Msikiti wa Kale" na ulijengwa kati ya karne ya 11 na ya 12. Inadhaniwa kuwa kulikuwa na msikiti mwingine chini yake kabla ya huu kujengwa, kwani mashimo ya nguzo za miti yalipatikana chini ya mihrabu. Usanifu wa msikiti huu unaonyesha kwamba badala ya kuba, msikiti huu ulikuwa na paa la gorofa. Vipengele vingine vya usanifu ni maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya kuweka kitabu kitakatifu (Qur’ani) na masanduku ya mafuta ya jadi. Na kama misikiti ya kisasa, Kibra imeelekezwa kuelekea Makkah. Fikiria jinsi vipengele hivi muhimu vya usanifu vilivyoonyeshwa hapa Kilwa vimeendelea kuwa sehemu ya usanifu wa Kiislamu hadi leo, miaka 800 baadaye.
Mzee Said Hamisi
Alama zilizokuwepo misikiti hii ya sasa hivi, ina utofauti mkubwa na ujenzi wa misikiti ya zamani. Misikiti ya zamani mingi ilikuwa juu haina bati, lakini sasa hivi ina bati kuna yale matungi yale kama ni mapambo sasa hivi hakuna. Na zamani ilikuwa nguzo zinakuwa nyingi zaidi misikiti ya zamani yote, nguzo zinakuwa nyingi kuliko misikiti ya sasa hivi.
Abdalla Ahmadi
Aina ya malighafi au nyenzo ambayo ilitumika, walitumia mawe ya matumbawe, walitumia udongo mwekundu, mchanga mweupe, chokaa bila ya kutumia nondo wala simiti. Kwa hiyo, tunakuta hawa watu walikuwa na teknolojia za hali ya juu, ndio maana tunakuta mpaka hii leo, unadumu kwa muda mrefu na mpaka hii leo kutokana na yale nyenzo waliyotumia, mpaka leo bado unaduma katika mandhari mazuri.
Stop 4. Upanuzi wa biashara na muundo
Upanuzi wa Msikiti Mkuu ulifanywa na Sultani Ali Hassan Bin Suleiman mwaka 1320, kufuatia ukuaji wa jamii ya eneo hilo na kuwasili kwa wageni kutokana na ukuaji wa biashara. Msikiti ulijengwa kwa muundo wa usanifu wa kipekee na wa kipevu, ukiwa na nguzo 42 na kuba 36. Wakati huo, ulikuwa msikiti mkubwa zaidi barani Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara. Msikiti huu ni ishara ya ukuaji wa tamaduni za Kiswahili na utajiri wa Kilwa kama bandari maarufu ya biashara. Sababu hizi pia zilichangia kuenea kwa Uislamu Afrika kutokana na mwingiliano wa wageni wengi, hasa wafanyabiashara, wenyeji mashuhuri, na mchunguzi maarufu Ibn Battuta, ambaye aliwahi kusema kwamba Kilwa ilikuwa ni mji mzuri zaidi aliowahi kutembelea.
Revocatus Weja Bugumba
ukaongezwa pale 13, 14 ambapo sasa wakati ndio Kilwa inakuwa sasa iko kwenye kilele cha mafanikio ambacho ndio kilikuwa ni himaya ilikuwa inatawala ukanda wote wa Afrika Kusini mwa Sahara, lakini upande wa bahari ya Hindi visiwa vyote vilikuwa chini ya himaya ya Kilwa Kisiwani ambacho kipindi hicho licha ya kwamba ilikuwa inatengeneza fedha zake za mwanzo za shaba, lakini kipindi hicho ndio inatengeneza fedha zake ambazo zimenakishiwa kwa dhahabu, kuonyesha kwamba ilikuwa ndio imefika kwenye kilele chake ambapo ndio wakaujenga na huo msikiti mkuu ulijengwa inawezekana kwa sababu ya watu kuongezeka lakini pia uchumi kukua. Na ndio maana ukiangalia majenzi yake yanaonyesha ya kwamba watu walikuwa na fedha. Unaweza kuangalia ni kidogo lakini uchongaji wako ukitafsiri kwa pesa sasa hivi, kwa pesa sasa hivi huu msikiti labda tunauchonga tunajenga, sidhani kama utashuka chini ya bilioni moja kujenga pale. Lakini sasa ungekuwepo nadhani ni msikiti ungekuwa kwa ukamilifu wake sasa hivi tukiangalia thamani yake unaweza hata karibia bilioni 10, kwa jinsi ya thamani ya sasa hivi. Lakini kwa sasa tupate tu mbao lenyewe unajua tu mbao moja kulipata, kulichonga tu fundi mwenyewe alichonga na uithaminishe na muda wake, unajua ni jengo la thamani sana. Kwa hiyo ni alama ni kwamba walitumia hiyo kulikuwa na mabadiliko na kuwa kwa uchumi wake.
Mercy Mbogelah
Biashara kwa ujumla ina mchango mkubwa kwenye ujenzi wa msikiti mkubwa. ukiacha ujenzi wa msikiti mkubwa biashara yenyewe kwenye ukuaji wa mji wa kilwa kisiwani ina mchango mkubwa, kwa sababu Kilwa ilikuwa kituo kikuu cha biashara, kwenye ukanda wa pwani ya Afrika Mashariki tangu karne ya kumi na mbili mpaka karne ya kumi na sita, biashara imekuwa na mchango mkubwa sana kwenye ukuaji wa mji wa Kilwa Kisiwani. Lakini Biashara ndio iliowafanya wafanya biashara wakubwa waingie kwenye mji huu wa Kilwa, na watu walipokuwa wakiongezeka, kwa maana wafanyibiashara mbali mbali maarufu walipokuwa wakiongezeka, ilipelekea sultani wa kipindi hicho aone sababu ya kuujenga msikiti mkubwa wa Kilwa Kisiwani, ili iwe rahisi wafanyibiashara hawa, pamoja na hawa watu maarafu waliokuwa wanaishi Kilwa Kisiwani, waweze kufanya swala ndani ya msikiti mkubwa. Kwa hivyo utaona biashara ilipokuwa inakuwa, ilikuwa ni sababu ya ongezeko la watu wafanyibiashara mbalimbali, na ndio iliyopelekea ongezeko lile la watu msikiti mkubwa uweze kuongezwa.
Mzee Said Hamisi
Kwenye msikiti mkubwa, kwenye msikiti mkubwa alama zake ule kwanza, una sehemu mbili, ambazo mwanzo ulikuwa mdogo, baada ya kuongezeka mahitaji ukaongezwa tena sehemu ya pili. Kwa hio ina kibla mbili, ndio maana unaitwa unaitwa ule msikiti wa kiblatena. Kwa hio misikiti ya sasa hivi kiti iko ambacho huezi kukuta, lakini ule umekuwa hivo na sababu zake ni hizo, kuongezeka kwa mahitaji basi ukaundwa kuja huku nyuma.
Abdalla Ahmadi
Ibn Battuta ni Morocco ambaye yeye alifika hapa, mwaka ya elfu moja mia tatu thelathini na moja sawasawa na karne ya kumi na nne. Yeye alifika hapa kuchangia kikubwa moja biashara, na utembeaji wake alitembelea karibu miji mia moja au zaidi, unakuta kwanza daksheni ni mzuri inang'aa inapendeza. Wenyeji walimpokea kwa ustaarabu wa juu na unyenyekevu, kwa historia ya kuwa nchi ya Kilwa ilikuwa wenyeji wa hapa wana ustaarabu wa hali ya juu, lakini pia alichangia ukuaji wa lugha ya Kiswahili, kutokana na hii nchi ya Kilwa Kisiwani moja ikiwa ni chimbuko ya lugha ya Kiswahili, kwa hivyo hata yeye ukuji wake aliweza kuchangia zaidi lugha ya Kiswahili, pia na kibiashara kukuwa zaidi.
Stop 5. Mapambo ya usanifu
Usanifu na mapambo ya msikiti mpya yanaonyesha uhusiano wa kihistoria wa Kilwa na biashara, kwani wafanyabiashara kutoka sehemu mbalimbali walileta bidhaa kadha wa kadha, zikiwemo sahani, vikombe, na vyombo vya udongo ambavyo vilijumuishwa katika muundo wa jengo hilo. Ndani ya kuba kulikuwa na vikombe vya porcelaini vya rangi nzuri na ambavyo vilivyopambwa kwa ustadi ambavyo vilitoka Arabia na China. Jaribu kufikiria uzuri wa kuba wakati msikiti ulikuwa katika kilele chake. Muonekano tofauti wa kila kuba unachangia msikiti huu kuwa wa kipekee kabisa. Kuna aina mbili za kuba zinazozungumziwa katika msikiti huu: kuba za mviringo na kuba mfano wa pipa. Kuba zaa mviringo yanatumika hasa kama maumbo ya kimapambo.
Mercy Mbogelah
Kwa kweli ninapenda maeneo makubwa mawili kwenye msikiti mkubwa. Eneo la kwanza ninalopenda ni Mitungi au Kuba za msikiti mkubwa, na kwa namna zilivyopambwa kwa mapambo ya aina mbalimbali, ni kitu ambacho ninapendezwa nacho. Lakini pia ninapenda kwa namna msikiti mkubwa ulivyopambwa kwa zile nguzo, ambazo ni nyingi ukizihesabu ni kama zinafika arubaini, arubaini na mbili. Kwa hivyo namna zilivyopambwa na zile nguzo, ni vitu ambavyo ninavifurahia ninapoingia ndani ya msikiti mkubwa.
Mzee Said Hamisi
Umuhimu wake unaweza kusema ni kuonesha tu utaalamu wa zama hizo, na zama hizi ambazo tuko nazo sisi. Kwa sababu wakati huo tunasema teknolojia ilikuwa iko chini sasa hivi imeongezeka zaidi. Lakini wao walikuwa wana uwezo wa kufanya vitu bora zaidi kuliko sasa hivi, vitu imara zaidi kuliko sasa hivi.
Abdalla Ahmadi
Kuba ina umuhimu wake mkubwa kwa sababu ule ni msikiti mkuu, na ilijengwa vile kuonyesha jinsi ya ukubwa iliopo, uliopo ule msikiti pia daraja au vyeo ambayo walikuwa wanatumia wale masheikh maimam kadhalika waumini mbalimbali. Kwa hivyo ule pale ile kuba kubwa kuonyesha jinsi ya mandhari ule vile ulivyojengwa kutokana na mandhari yake hali ya kuwa ni mzuri unapendeza kwa hivyo wakaeka yale kuba kubwa kuonyesha wana uwezo zaidi wa kujenga katika hali nzuri kama ile.
Stop 6. Maoni tofauti
Mbali na eneo kuu la ibada, lenye kuba ndogo na nguzo nyingi za Msikiti Mpya, kuna kuba moja kubwa na maeneo mawili ya kuutawazia. Katika eneo la kutawaza ambalo waumini wengi walikuwa wakilitumia, visima vya kale vyenye umuhimu wa kiroho vilikuwa vikitumika kujaza makaro ya maji. Kuna visima vingi vya kale, lakini kisima kikuu ndicho pekee kinachobeba maji safi. Inasemekana kwamba wale wanaotumia maji haya hadi leo hupokea baraka, ulinzi dhidi ya shida, na faraja kutokana na taabu. Eneo chini ya kuba moja kubwa kuna mkinzano wa mawazo baina ya wasomi na wanajamii. Wasomi wanaliita eneo hili kama mahali maalum alilotumia Sultan wakati wa sala. Hata hivyo, jamii ya wenyeji inasema kwamba kwa sababu Sultan alikuwa kiongozi anayeheshimiwa sana, asingeweza kukaa nyuma ya msikiti. Badala yake, wanasisitiza kwamba alifanya udhu katika eneo dogo lililotengwa kabla ya kuingia msikitini. Kisha alisali kwa faragha, au kutekeleza sala za Sunnah chini ya kuba kubwa, kabla ya kujiunga na umma kwa ajili ya sala kuu kwenye mstari wa mbele.
Revocatus Weja Bugumba
Pia kuna hizi kubwa kabisa ambayo iko tofauti, ambayo iko karibu na nchi lakini kubwa karibu na ule mti mkubwa ambayo ni kubwa ya aina yake. Hiyo kubwa kwa masimulizi ya watu wanahisi wanasema ule mlango alikuwa anapitia sultani na ndipo alikuwa anatawazia hapo kadri ya masimulizi kwamba labda ndio alikuwa anapita na anakaa pale lakini kwa tafsiri za wataalamu wa dini wanasema hawezi sultani akakaa kwa ile kubwa, kwa sababu kwa mujibu wa utamaduni wa ibada za kiislamu watu wakubwa ndio wanakaa mbele, mstari wa kwanza kule, na kama hayupo hata imamu yule mtu mashuhuri anaweza mwenyewe kuongoza ibada. Tuna mfano mzuri tulikuwa na mzee Ali Hassan mwenyewe hayati rais wetu wa kwanza, wa pili wa jamhuri ya Muungano wa Tanzania, alikuwa wakati mwingine pia anaongoza ibada katika shughuli za kiibada. Kwa hio, hio wazo ndipo alikuwa na kama Sultani linashindwa na utamaduni wa dini ya kiislamu. Lakini pia kuna watu wanaamini ni alama nyingine lina maana kwamba watu wanasema huwa kuna majini pale yanakaa. Kwa hivyo unaweza kukaa si majini ya sijui ni ya mapenzi au ni ya kitu gani lakini ndio wanakaa ndani ya hapo watu wanaamini watatuambia wataalam.
Stop 7. Juhudi za jamii za uhifadhi
Uhifadhi wa Msikiti mkuu ulianza tangu kipindi cha utawala wa mwingereza chini ya usimamizi wa mwanaakiolojia wa kwanza Neville Chittick ambaye alifanya uchimbuaji kwenye jengo lote la msikiti ili kuondoa kifusi na kukitupia baharini. Baada ya hapo uhifadhi uliendelea mwaka 2000-2004 na 2014 chini ya ufadhili wa UNESCO na World Monument Fund kwa kufanya ukarabati wa msikiti. Wanajamii hushiriki kwenye kazi za uhifadhi ambapo kupitia miradi mbali mbali kwa ufadhili wa kimataifa na wa ndani, wanajamii zaidi ya asilimia themanini walishiriki katika kazi za ukarabati aidha vijana zaidi ya thelathini walishiriki na kupata mafunzo ya uhifadhi na ukarabati wa majengo ya kale. Mafunzo hayo yalijumuisha utengenezaji wa chokaa, uchongaji wa nakshi na mawe maalumu ya ukarabati. Pia wanajamii vijana walipewa mafunzo ya namna bora ya kuongoza watalii.
Revocatus Weja Bugumba
Na ndio haya mabadiliko, lakini upande wa uhifadhi ulioanzia hasa mwaka wa '57 Historia inatuonyesha ya kwamba Neve Chikt ndio alikuwa mkurugenzi wa kwanza wa mambo ya kale kipindi cha wakoloni, kipindi cha muingereza. Kwa hiyo yeye alikuja na timu ya wanafunzi kutoka chuo cha Makerere ambao walikuwa wanasoma mambo ya urithi akiwemo mkurugenzi wa kwanza wa mambo ya kale anaitwa Amini, Marehemu Amini Mturi, wakiwa vijana ndio walishiriki katika kazi hizi pia pamoja na Chikt, ndio wakafanya kazi ya ukarabati ambao walifanya sio hapa tu kama alivyoeleza mzee Hassan waliondoka hapa wakafanya Husuni Kubwa na maeneo mbalimbali. Kwa sababu Chikt alifanya ukarabati maeneo yote kuanzia ukanda wa pwani kuanzia Tanga mpaka kusini mwa Tanzania. Lakini baadaye lakini miaka hiyo sasa wa '57 mpaka '60 alijikita kwenye eneo la Kilwa mpaka miaka '70 alikuwa anaandika kuna meza yake alikuwa ameacha hapa, meza ya Chikt, kama bado sijui kama mnayo, ile meza nilikuwa naitumia, ile meza ni ya Chikt. Kwa hiyo ndio alikuwa anatumia katika kuandika kwenye ofisi yake kwa hiyo mpaka miaka 70 alikuwepo lakini ndio akaanza kuandika hivi vitabu vyake. Lakini kutoka hio '70 baada ya miaka 70 hapakuwa na mwendelezo hata ukarabati, walikuwa wanafanya usafi tu wa mwaka, kwa mwaka ni usafi mpaka mwaka wa 2002, tulipopata mradi ambao unaitwa mradi wa Kilwa project ambao ulifadhiliwa na serikali ya Ufaransa pamoja na serikali ya Japani UNESCO na serikali yenyewe ya Tanzania. Na kazi hiyo iliyofanyika haikuwa tu ya ukarabati lakini ya kukarabana, ukukarabati wa msikiti mkuu kilichofanyika ni kuongeza nakshi kwenye zile vinara kuna sehemu ambazo ukienda kusoma pale imeandikwa 2002, 2004 zimeandikwa pale alama pale, ndiyo zilizoongezwa kipindi hicho kwenye msikiti mkuu lakini kwenye ndunzi nazo waliongeza, tuliongeza unene ili kuzuia maji yaliyokuwa yanazama. Kwa hizo kubwa zote ziliongezwa ambazo zilikuwa zinavuja sio kama zinaonekana nyeusi lakini kubwa ziliongezwa pia ukubwa na kusafisha pamoja na msikiti ambao tumekaa ukiangalia huu ndio msikiti wanafunzi waliohitimu kazi ya ukarabati, walifanyia mafunzo yao hapa na kupatiwa vyeti. Ulifanywa na wanafunzi kuonyesha kwamba wamehitimu mafunzo ya uhifadhi. Kwa hiyo uhifadhi wa mwisho ndio ulifanyika huo katika nyakati 2002 mpaka 2004 kwa msikiti.
Mercy Mbogelah
Msikiti mkubwa wa kilwa Kisiwani una mchango mkubwa katika jamii. Namba moja, kuna uhusiano kati ya msikiti mkubwa na imani ya wanajamii, kwa maana Uislamu. Kwa sababu, wapo wanajamii ambao mpaka leo wanautumia msikiti mkubwa kwa kuswali, wakiamini kabisa anapoingia kwenye msikiti mkubwa kuswali au kufanya swala, basi Mwenyezi Mungu anamsikia kwa sababu ya historia iliyopo ndani ya msikiti mkubwa. Lakini msikiti mkubwa pia kwenye swala la kiimani, vile vile unatumiwa na wageni mbali mbali kutoka nje ya kilwa, kwa maana mikoa mingine ya Tanzania lakini na wageni kutoka nje ya nchi. W anakuja kuutumia msikiti mkubwa kwa kuswali nje ya kutalii lakini wana swali pia. Kuna wageni kama makundi ya Waarabu kutoka Uturuki, Omani na kadhalika, huwa wanafika kila mwaka ni karibu miaka minne sasa kila mwaka wanafika kipindi cha ramadhani. Wanafanya swala pamoja na wananchi wote wa mji wa Kilwa Kisiwani, wanafuturu, wanafanya swala ndani ya msikiti mkubwa pamoja na kufutorisha. Kwa hiyo utaona ni kwa namna gani msikiti mkubwa una thamani wanaupa thamani, wananchi wa Kilwa Kisiwani lakini na wageni wa nje wa Kilwa kisiwani. Wageni wanaokuja kwenye mji wa Kilwa Kisiwani wanakuja kutalii. Wananchi wanajipatia vipato kupitia msikiti mkubwa, kwa sababu wapo waongoza watalii, ambao ni wenyeji wazawa wanaoongoza wageni kwenye mji wa Kilwa Kisiwani, kwenye msikiti mkubwa wanajipatia vipato. Waendesha vyombo vya baharini ambao wanawapakia wageni hao, nao wanajipatia vipato kupitia kuongoza wageni kwenye msikiti mkubwa.
Masoudi Issa Abeid
Msikiti mkubwa nilihifadhi, nilihusika kwa namna mbili hivi. Kwanza kutoa elimu, lakini pia kuyaangalia mandhari yenyewe ya maharibiko, labda pengine kwa wanyama na mifugo ya mbuzi ng'ombe kipindi kile tulikuwa tunahusika sana. Lakini pia tulihusika tena wakati yuko oyesco pamoja na mambo kale, na Mimi ndio nilikuwa kiongozi kipindi kile mwenye kiti wa kamati ile ya magofu, kipindi cha kwanza kabisa kabla kamati hii kwa hivyo nilihusika sana katika msikiti ule.
Mzee Said Hamisi
Kunufaika kwetu sisi mtu binafsi ukiamua wewe mwenyewe, kwamba niende nikapate baraka za pale basi ndio unanufaika. Lakini huezi jua kwamba labda manufaiko haya mimi kwa sababu ya kuenda pale, huezi jua kwa sababu hakuna anayekuambia, ila imani yako ndio inakujenga kwamba umenufaika kwa kupitia vitu vile.
Stop 8. Hitimisho
Msikiti una maana kubwa sana kwa wanajamii wanaoishi ndani ya Hifadhi na kwa wageni wenye matumaini ya kuabudu na watalii wanaohitaji kujifunza kuhusu magofu. Kwa wanajamii na baadhi ya wageni wenye imani ya kiislamu, msikiti ni mahali pa kuheshimiwa ambapo huweza kusali kwa Mwenyezi Mungu na msikiti huo kuungana na wazee wao waliopita ambao wanamahusiano ya karibu na eneo hili. Wengi wao huamini kuwa maombi hayo huwasaidia kuwakinga na na mikosi, laana na majanga ya aina mbalimbali. Vilevile wageni wanapotembelea msikiti huo hupata fursa ya kujifunza na kufahamu historia yake na pia kutambua mchango wa kisiwa katika kuenea kwa tamaduni za kiisalamu na kiswahili.
Revocatus Weja Bugumba
Mimi kama mtaalam wa mambo ya kale kwa sababu tunachokitunza, kwanza ni ile akili iliyotumika. Mambo ya kale hatutunzi kwa sababu tu ya ukale wake, lakini ni ile akili, ubunifu na usanii uliotumika kukifanya kile kitu kikiwepo. Ni vile vile kama vile husema mzee Hasani ni kwamba yaani ni, watu walitumia ustadhi wa hali ya juu kutengeneza na kujenga lile jengo. Kwa hiyo kwangu mimi msikiti mkuu ni eneo ambalo linatuonyesha ubunifu wa hali ya juu sana, na uwezo wetu wa kutumia akili kama tunavyopaswa kuvitunza vitu vingine ambavyo ndio lengo letu, mambo ya kale, mambo ya kale sio tunasema kwa ukali, hapana, ni akili iliyotumika kubuni hata lile jiwe tunalitunza sio kwa sababu ile akili ilitotumika kulichonga lile jiwe. Lakini ina historia yake pia umuhimu wake akili na historia yake. Historia yake ndio tunasema kwamba ni msikiti wa kwanza kwa wakati nilivyoeleza mwanzoni katika ukanda wa zanzibar na pia ni mkubwa sifa zake hizo. Kwa hivyo na hizo sifa zote, zinaifanya msikiti uwe ni tuseme ni nembo yetu kuu ya ya hapa Kilwa kisiwani
Mercy Mbogelah
Ninafikiria, endapo tutaendelea kuhifadhi mji wa Kilwa Kisiwani, magofu ambayo tunayaona hivi leo yanaweza yakadumu kwa miaka elfu moja zaidi, kwa sababu hivi leo tunavyoyaona ni kwamba yalihifadhiwa, hata wanajamii waliokuwepo miaka 50 iliyopita tangu miaka na miaka, walikuwa na roho ya uhifadhi na walisaidia sana katika kuyahifadhi, na ndio maana leo hii tunayaona na tunaona namna ambavyo yanatunufaisha, yananufaisha jamii, serikali kwa ujumla, taifa kwa ujumla linanufaika kupitia hifadhi ya magofu ya Kilwa Kisiwani. Kwa hiyo ni matumaini yangu kwamba wananchi kwa kushirikiana na serikali, na wadau mbalimbali wa uhifadhi kutoka nje ya taifa la Tanzania, tukishirikiana kwa pamoja kuyalinda, kuyahifadhi, kuyakarabati, tunaweza tukaendelea kutunza urithi wa kitaifa, urithi wa kimataifa ukadumu vizazi ukanufaisha vizazi na vizazi.
Masoudi Issa Abeid
Unafaa kuwa kwa kwanza kabisa tunakuwa na heshima kwa urithi wa dunia, hilo linatuheshemisha sana kuwa na vitu kama hivi na vimeingia katika urithi wa dunia. lakini hata vile sasa hivi tunanufaika hata kipato cha mtu mmoja mmoja, kutoka katika miaka iliyopita mpaka sasa hivi, imekuwa tofauti kidogo sasa hivi hata watu mmoja mmoja wanaanza kuona manufaa, kama vile mtoto mmoja mmoja anachukuliwa anasomeshwa kwa sababu ya rasilimali hizi. Lakini hata vilevile tunakuwa na elimu tunakuwa na washa, lakini kina mama vilevile wanakuwa na kundi muda mwingine, wanapika vyakula vya asili lakini hata vilevile UNESCO ilitupa mafunzo mengi kipindi kile ya mambo ya upishi wa vyakula vya kienyeji, mambo ya ngoma, mambo ya vikoba, walichukua UNESCO wakapitia kesi rahisi tukashughulika nao kiasi asilimia themanini na tatu. Tulifanikiwa sana kwa hio hayo bado ni manufaa makubwa na tunaendelea nayo, lakini pia kuna vijana wanaojihadhiri kuvuja wageni kwa boti zao binafsi hizo pia ni ajira, lakini tunatoa gaidi wote wana asili ya hapa na hao wanatembeza wageni, hiyo yote ni manufaa na wakati wa zamani ilikuwa hakuna hayo.
Mzee Said Hamisi
Mimi najiskia faraja sana na pia ninaweza nikaenda pale, nikafanya ibada yangu kwa kutafuta ile baraka ya wakubwa wale waliopita, basi baraka ile na sisi tuendelee kupata, unaweza ukaenda pale ukasali la kateni au siku ingine ukasali ya adhuhuri au la asili pale, kupata baraka za wale wakubwa na baraka za ile misikiti.
Abdalla Ahmadi
Kubwa ambalo nalielezea hapa juu ya kuyahifadhi, kuyatunza ilimradi yakuwe kama tulivyo kauli mbio tumeris na tuarisishe, kwa maana ya kuwa moja kwa moja iwapo itakuwa tutaacha kuvitunza, na kuvihifadhi zaidi inamaana tutapoteza hali ya uhalisia, kwa hivyo ni vitu vizuri ya kuweza kuvitunza, ya kuweza kuvienzi ya kuweza... Ili yakuwe katika mandhari mazuri kama tulivyovikuta, na tuweze tuwaachie hao ambao wanakuja.